KCSE KISWAHILI 102/1_Makala ya Insha

TAHARIRI

  • Tahariri ni makala yanayotolewa katika vyombo vya habari yakieleza kuhusu swala fulani katika jamii.
  • Mara nyingi huwa ni swala fulani lenye umuhimu wa kijamii, kisiasa, kiuchumi, kitaifa, kimataifa na kadhalika.
  • Huonyesha waziwazi msimamo wa chombo fulani cha habari na swala husika pia hutoa mapendekezo kuhusu namna ya kutatua swala husika
  • Huonyesha namna swala hilo lilivyo tatizo au muhimu kwa jamii.

 

MUUNDO

  1. Anwani– mfano: TAHARIRI KUHUSU UFISADI HUMU NCHINI
  2. Aya tangulizi– kutoa maelezo mafupi kuhusu swala rejelewa/ jadiliwa. Kwa kuonyesha umuhumu wake/namna ilivyo tatizo/ namna inavyoshughulikiwa na kama juhudi hizo zinafanikiwa au la.
  3. Mwili- Hii ndiyo sehemu inayojibu swali. Hoja mbalimbali kuhusu swala jadiliwa zitolewe huku zikibainisha vizuri msimamo wa makala husika.
  4. Aya tamati-Inaweza kuwa muhtasari wa tahariri/ushauri wa kijumla.

Zoezi

Andika tahariri kuhusu juhudi za serikali kuimarisha sekta ya elimu nchini Kenya.

TAHARIRI KUHUSU JUHUDI ZA KUIMARISHA SEKTA YA ELIMU NCHINI

Elimu ni sekta muhimu humu nchini. Ni wazi kuwa waja wengi, wakubwa kwa wadogo wanategemea elimu ili waweze kutosheleza mahitaji ya ya maisha ya usoni. Aidha elimu inakumbwa na changamoto chungu nzima. Kwa mfano, kuna wizi wa mitihani, upungufu wa walimu na wanafunzi hasa wale wa kike, kuwepo kwa karo zisizoweza kulipwa. Serikali inafanya bidiikuhakikisha kuwa shida hizi zimeshikwa katika kaburi la sahau kwa kukabiliana nazo kwa jino na ukucha. Nina uhakika juhudi za serikali zitafua dafu.

Wizi wa mitihani hasa ule wa kidato cha nne umekita mipaka. Miaka zilizopita kuna baadhi ya shule zilizofungwa kwa sababu ya jambo hili. Serikali nayo kupitia wizara ya elimu imekabiliana na shida hii kwa kuwapiga kalamu viongzi ambao walikuwa wanasimamia elimu, walimu katika shule zilizopatikana na hatia, kuhakikisha kuwa mtihani umewekewa ulinzi ipasavyo. Juhudi hizi zimefua dafu kwani mwaka uliopita hakuna mwanafunzi aliyepata mtihani wakati usiofaa. Aidha, serikali inafaa kuwahimiza walimu kumaliza silabasi kwa wakati unaofaa ili kupunguza kesi za wizi wa mtihani, kwani wanafunzi watapata nafasi ya kudurusu kabla ya mtihani kufika.

Pili, Tume ya usajili wa walimu imeanza kuwasajili walimu baada ya kila miezi miwili ili kufidia upungufu wa walimu shuleni. Baadhi ya shule humu nchini wanafunzi huishia kubaki nyuma kimasomo kwa sababu ya upungufu wa walimu. Inadhihirika kuwa wengi wao huacha kazi kwani wao huhofia kutolipwa kwa wakati na hata kulipwa mishahara duni. Ningependa kuishauri serikali kuwa inafaa kuhakikisha kuwa mishahara ya walimu imelipwa kwa wakati na iwe ya kutosheleza mahitaji yao. Hili litawapa motisha walimu kwani hawawezi kufanya kazi bila malipo.

Aghalabu watoto wa kike huishia kuwa kitega uchumi. Wao huolewa ili wazazi wao wanufaike badala ya kupelekwa shuleni. Mara nyingi kesi hizi hutokea hasa katika maeneo ambayo hayajaimarika kiuchumi. Serikali imeweza kupambana na shida hii kwa kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi na wanajamii wanaowanyima watoto haki yao ya kupata elimu. Wazazi hao wanafaa kuelezwa jinsi elimu inaweza kumfaidi mtu. Kwa sasa asilimia sabini ya watoto hasa wale wa jinsia ya kike wanapata elimu bora. Haya yote yamefanikishwa na wizara ya Elimu.

Kwa kawaida mwanafunzi hawezi elimishwa katika mazingira mabovu. Mazingira yenye utulivu na vifaaa maalum vya ufunzaji vinafaa kuwepo ili masomo yawe yenye mafanikio. Serikali imeanza kujenga madarasa katika maeneo ambapo wanafunzi wanafunzwa kivulini. Aidha imeweza kusambaza vifaa kama vile vitabu, kalamu, chaki na hata vifaa vya kuchezea kama vile mipira. Tendo hili litamwezesha mwalimu na mwanafunzi kushirikiana vyema darasani na hata ya wanafunzi katika maeneo yaliyolegeza kamba katika ukuaji wa uchumi umeongezeka. Serikali inazidi kusambaza vifaa maalum vinavyohitajika ili kunafinisha elimu.

Elimu ya bure pia imewauni watu wengi mno. Hapo awali wazazi wengi hawakuwa na uwezo kulipa karo. Hali hii iliwafanya wengi wasipate fursa ya kuelimishwa. Ukilinganisha idadi ya wale waliojiunga na shule mbalimbali, utagundua kuwa wengi hawakuweza kuingia shuleni kwa sababu ya ukosefu wa karo. Hongera kwa serikali kwani watoto wanaweza kujiunga na shule waitakayo bila kuwepo kwa vizuizi.

Wanafunzi wanafaa kushauriwa mara kwa mara. Hali hii humpa mwanafunzi utulivu anapokuwa darasani na kumwesheza kuepukana na tabia ambazo zitamfanya asiwe makini darasani. Isitoshe wanafunzi huweza kupewa maarifa yatakayotumiwa kutatua shida zinazowakumba wao wenyewe. Serikali imefanikisha hali hii kwa kuwaajiri washauri nasaha na kuwajengea ofisi zao humo shuleni. Kwa hakika matunda ya juhudi hii ni mazuri sana.

Tamasha mbalimbali huandaliwa na hata michezo miongoni mwa shule kadhaa. Utagusano baina ya wanafunzi wa shule tofauti tofouti huwezesha mbadilishano wa maarifa baina ya wanafunzi. Jambo hili humfanya mtu awe mwenye busara na hekima nyingi itakayomsaidia katika maisha ya usoni. Aidha hali hii pia humpa mwanafunzi fursa ya kumpumzisha akili baada ya kusoma kwa muda mrefu.

Hatimaye, tunafaa tushirikiane na serikali katika juhudi za kuimarisha elimu nchini. Aidha, serikali imeweza kupambana na changamoto tofauti ili kufanikisha sekta ya elimu. Sote kama wananchi tunafaa kujitoa mhanga ili elimu iwe bora zaidi.

Leave a reply

Start a conversation.
Hi! Click on one of our members below to chat on WhatsApp.
The team typically replies in minutes.